-

Ini lako, afya yako

Kwa nini ini lako ni muhimu

Karibu kila kitu unachokula na kunywa hupitia kwenye ini. Hata kemikali zinazogusa ngozi yako na sumu unayovuta hewa yake hupitia kwenye ini lako.
Ini lako lina kazi nyingi muhimu za kufanya mwili wako uendelee kufanya kazi ipasavyo. Kati ya kazi hizi muhimu ni kuondoa sumu mwilini mwako na kubadilisha virutubishi kwenye chakula kuwa nguvu. Hata hivyo, ini lililoharibika haliwezi kufanya kazi hizi ipasavyo, kwa hivyo ni muhimu kudumisha afya ya ini lako.

Ukweli kuhusu ini

 • ni ogani kubwa zaidi ya ndani ya mwili
 • linapatikana upande wa kulia wa kiwiliwili chako, nyuma ya mbavu zako
 • linaweza kujikarabati lenyewe na kutengeneza tishu mpya za ini zenye afya
 • seli za ini huvunjavunja mafuta na kutoa nguvu mwilini
 • lita 1.5 za damu hupita kwenye ini lako kila dakika

Mtu yeyote anaweza kupata ugonjwa wa ini

Kuna magonjwa mengi ya ini ambayo yanaweza kuathiri watu wakubwa na watoto. Watu walio katika hatari ya ini kuharibika ni pamoja na watu ambao:

 • wana uzito kupita kiasi au wanene sana na wana ini lililojaa mafuta
 • hunywa pombe kwa wingi
 • wana maambukizi ya virusi ambayo hayajatambuliwa au kutibiwa kama vile Homa ya manjano ya B au Homa ya manjano ya C
 • wana tatizo la mfumo wao wa kinga ya mwili ambalo husababisha ugonjwa wa ini
 • huzaliwa na ugonjwa wa ini

Homa ya manjano ni nini?

Homa ya manjano inamaanisha kuvimba kwa ini. Ini lililovimba wakati mwingine hupanuka au kufura. Sababu za kuvimba kwa ini zinaweza kujumuisha maambukizi ya virusi vya Homa ya manjani kama vile Homa ya manjano ya B au Homa ya manjano ya C, pombe, dawa au mafuta. Wakati mwingine kunaweza kuwa na mchanganyiko wa hali hizi.

Kutambua dalili

Ini lililoharibika linaweza kuendelea kufanya kazi kwa muda mrefu bila kuonyesha dalili au ishara za kuharibika. Isitoshe, baadhi ya dalili za ugonjwa wa ini zinaweza kukosa kutambuliwa kwa sababu zinafanana na za ugonjwa wa kawaida. Hatua salama zaidi ya kuchukua ni kuzungumza na Daktari wako wa Matibabu ya Jumla wa eneo (GP), Mtaalamu wa Afya, Muuguzi Aliyehitimu (NP) au Muuguzi wa Tiba ya Ini ikiwa una wasiwasi kuhusu dalili zozote zifuatazo:

 • unajihisi kuwa mgonjwa na mchovu kila wakati
 • unahisi maumivu au ulaini katika sehemu ya mwili ambapo ini linapatikana au kwenye eneo lote la tumbo
 • kuwashwa mwili wote, hasa usiku
 • kuvimba kwa vifundo vya miguu
 • Ngozi kuwa ya rangi ya manjano (ngozi na macho ya manjano)
 • hali isiyo ya kawaida au isiyokoma ya kukojoa mkojo mweusi
 • kuchanganyikiwa au kuhisi kuwa na wasiwasi

Nenda ufanyiwe ukaguzi wa ini

Kadri unapotibu chanzo cha uharibifu wa ini mapema, ndivyo unaongeza fursa ya
kuboresha afya ya ini lako. Mwombe GP wako akague ini lako ikiwa una wasiwasi.

Ukaguzi wa ini ni nini?

Ukaguzi wa ini kwa kawaida hufanywa kwa kutumia vipimo vya damu ambavyo hupima jinsi ini lako linavyofanya kazi. Matokeo husaidia GP kuchagua vipimo vingine vya kufanya. Vipimo hivi vinajumuisha:

Kupiga Picha ya Ini/Ndani ya Tumbo

 • hutupatia maelezo kuhusu ini na husaidia kutuonyesha iwapo ini liko katika hali ya kawaida au iwapo uchunguzi wa ziada unahitaji kufanywa.
 • Gharama ya Kupiga Picha ya Ini/Ndani ya Tumbo hulipwa na Mpango wa Bima ya Medicare (Medicare Benefits Scheme (MBS)). Utarejeshewa pesa zote za matibabu ulizolipa ikiwa una kadi ya bima ya Medicare.

FibroScan

 • picha ya kitaalamu ambayo hukadiria mabaka kwenye ini lako.
 • Unaweza kupata huduma ya FibroScan bila malipo kwenye Kliniki za Umma za Matibabu ya Ini kwa Wagonjwa Wasiolazwa. Kliniki za kibinafsi zinaweza kutoza huduma ya FibroScan na HUTAFIDIWA pesa ulizotumia na Medicare.

Vidokezo halisi vya kuendelea kuwa salama

Dhibiti matumizi yako ya dawa

Tumia tu dawa zilizoagizwa na GP, Mtaalamu wa Afya, Muuguzi Aliyehitimu au Daktari wa Tiba ya Akili wa eneo lako. Usipitishe dozi iliyoagizwa. Usitumie dawa zilizoagizwa pamoja na pombe na/au dawa za kulevya. Dawa zingine zikitumiwa kwa kipimo cha juu zinaweza kuwa sumu kwenye ini lako (kama vile paracetamol).

Punguza au acha kunywa pombe

Kadri unavyopunguza unywaji wa pombe, ndivyo unapunguza hatari ya kupata madhara yanayotokana na pombe.

Acha kuvuta sigara au bangi au dawa zingine za kulevya.

Sumu na kemikali zilizo kwenye sigara zinaweza kudhuru ini lako. Matumizi ya kipimo cha juu cha bangi yanaweza kuongeza uharibifu wa ini. Kuna hatari ya kupata kansa ya ini ikiwa unatumia sigara au bangi.

Tumia mbinu salama ya kujidunga

Tumia kifaa safi na chako mwenyewe cha kujidunga. Ikiwezekana, nenda kwenye chumba kinachosimamiwa cha kujidunga. Usiwahi kamwe kushiriki kifaa cha kujidunga.

Kuwa makini na kujichora chale na kujidunga mwilini

Chagua kituo ambacho kinafuata mwongozo wa Uzuiaji wa Maambukizi, tumia sindano za kutumiwa mara moja na wino uliotakaswa.

hiriki katika ngono salama

Tumia kondomu wakati wa kufanya ngono kupitia uuke, mdomo na mkundu. Hatua hii itakulinda dhidi ya kupata maambukizi ya virusi kupitia majimaji ya ngono au damu.

Dumisha usafi wa kibinafsi

Vitu ambavyo vinaweza kuwa na kiasi kidogo cha damu (mswaki, wembe), havipaswi kushirikiwa. Tupa vitu vilivyo na damu inayoonekana kwenye mfuko uliofungwa na uweke kwenye biwi la taka.

Mipango ya Usafiri

Hali ya kusafiri katika nchi zingine inaweza kukuweka katika hatari ya kuambukizwa virusi vya Homa ya manjano ya A. Zungumza na GP wako kuhusu chanjo na utumie maji ya chupa au yaliyochemshwa katika safari yako.

Pombe hushinikiza ini lako
Ili kupunguza hatari ya kupata madhara kutokana na majeraha au magonjwa yanayohusiana na unywaji wa pombe, wanaume na wanawake wenye afya hawapaswi kunywa zaidi ya vinywaji 10 vya pombe ya kiwango cha wastani kwa wiki na vinywaji vya pombe ya kiwango cha wastani visivyozidi 4 kwa siku. Kinywaji kimoja cha pombe ya kiwango cha wastani kina 285mls cha nguvu kamili ya bia (4.9% alc/vol). Kadri unavyopunguza unywaji wa pombe, ndivyo unavyopunguza hatari ya kupata madhara yanayohusiana na pombe. (NHMRC ، 2020).

Hatua za ugonjwa wa ini

Kuna aina nyingi za ugonjwa wa ini ambazo zinaweza kusababisha kuendelea kuharibika kwa tishu za ini lako. Ugonjwa wa ini unapotambuliwa mapema, unaweza kutibiwa mapema. Ugonjwa wa ini unaoachwa bila kutibiwa unaweza kusababisha utendakazi duni wa ini au ini kuacha kufanya kazi. Kuendelea kwa ugonjwa wa ini hutofautiana kulingana na chanzo chake. Kuvimba kwa ini kunaweza kuchangia kutengenezwa kwa tishu iliyoharibika (fibrosis). Uvimbe unaoendelea unaweza kusababisha kuharibika zaidi kwa tishu ya ini (cirrhosis). Kuwepo kwa tishu iliyoharibika zaidi huongeza hatari ya kupata kansa ya ini na kunaweza kusababisha ini kuacha kufanya kazi.

Kuvimba

Kunaweza kusababishwa na maambukizi ya virusi, pombe, matatizo ya mfumo wa kinga ya mwili, sumu, mafuta au mchanganyiko wa vitu hivi. Kuondoa au kutibu vyanzo hivi kwa kawaida husababisha kutoweka kwa uvimbe.

Fibrosis

Kutengenezwa kwa tishu iliyoharibika kwenye ini. Tishu ya ini ambayo imeharibika kiasi inaweza kupata nafuu na kupona.

Cirrhosis

Kuharibika kabisa kwa ini ni ugonjwa wa ini ambao hauwezi kutibiwa ambapo tishu yenye afya ya ini huharibika kabisa. Ini lililoharibika kabisa huwa gumu, lenye uvimbe na mara nyingi hupungua kwa ukubwa. Mara nyingi kazi ya ini huathiriwa vibaya zaidi. Matibabu yanaweza kuzuia ini kuharibika zaidi, kulinda tishu yoyote yenye afya ya ini iliyosalia na kurejesha baadhi ya kazi za ini. Utendakazi wa ini hubadilikabadilika katika hatua ya Cirrhosis.

Kansa ya ini

Kuharibika zaidi kwa ini huongeza hatari ya kupata kansa ya ini. Kansa ya ini inaweza kutibiwa kwa ufanisi ikiwa itatambuliwa mapema. Isipotibiwa, kansa ya ini inaweza kusababisha ini kuacha kufanya kazi.

Ini kuacha kufanya kazi

Ini kuacha kufanya kazi ni wakati ambapo ini hukoma kufanya kazi. Hii ni hali inayotishia maisha na inahitaji matibabu ya dharura. Watu wengine huenda wakahitaji kubadilishwa kwa ini.

Kuzungumza kuhusu wasiwasi wako

Ikiwa una wasiwasi wowote kuhusu ini lako, tafadhali zungumza na GP au Muuguzi Aliyehitimu wa eneo (NP). Mtoa huduma wako wa afya anaweza kuagiza vipimo vifanywe ili kutathmini utendakazi wa ini lako. Unaweza kuagiziwa dawa kulingana na matokeo ya vipimo. Dawa nyingi hulipiwa na Mpango wa Bima ya Dawa (PBS). Uchunguzi mwingi wa rediolojia kama vile kupiga picha ya ini hulipiwa na Mpango wa Bima ya Medicare (MBS). GP au NP wa eneo lako anaweza pia kukuelekeza umwone Mtaalamu wa Tiba ya Ini.

Jaribu kuzungumza na marafiki na wanafamilia ili upate msaada halisi na wa kihisia. Unaweza pia kuzungumza na watoa huduma wengine wa afya – ikiwa ni pamoja na wauguzi,
washauri, matabibu, wauzaji wa dawa au wataalamu wa lishe.

Msaada huleta mabadiliko makubwa

Unaweza kuhisi upweke na matibabu yanaweza kukufanya uhisi uchovu na mwenye wasiwasi, kwa hivyo msaada wa kihisia ni bora zaidi.
– Grenville, umri wa miaka 56

Watoa huduma za afya huleta mabadiliko makubwa

Ni kutokana na mtazamo wao. Nikiwa mgonjwa, mimi hutaka kwenda na kusikilizwa na kueleweka.
– James, umri wa miaka 56

Kudumisha afya ya ini lako

Programu ya LiverWELL ni programu ya simu ambayo ni rahisi kutumia ambayo inakusaidia udhibiti afya ya ini lako. Ina zana na vidokezo vingi vya kukusaidia kudumisha afya ya ini lako ikiwa ni pamoja na:

 • Kuweka vikumbusho vya kutumia dawa
 • Kuratibu miadi
 • Kurekodi na kufuatilia matokeo ya vipimo
 • Kuhifadhi madokezo

Unaweza kupata maelezo yaliyosasishwa kuhusu afya ya ini katika programu ya LiverWELL kama vile lishe bora, kuchangamka, kuwa mzima na kuzingatia vinywaji unavyotumia.

Kupata usaidizi

www.cancervic.org.au
www.betterhealth.vic.gov.au

Tutumie barua pepe katika info@liverwell.org.au
Piga simu kwenye LiverLine: 1800 703 003

Maelezo haya ni ya jumla na hayakusudiwi kutumiwa kama ushauri wa matibabu. Wasiliana na mtaalamu wa afya ili upate maelezo zaidi.

LiverWELL acknowledges the support of the Victorian Government.
We welcome people from all cultures, nationalities and religions. Being inclusive and providing equitable services is our commitment.

ABN 48 656 812 701

We acknowledge the traditional owners of the lands where we work - the lands of the Woi-Wurrung Wurundjeri people of the Kulin Nations. We express our gratitude to them for their continued care and curation of these lands and waters. We pay our respects to Elders past and present.

LiverWELL observes and honours the Kulin Nation's intrinsic connection to land, sky and water, and the creator Bunjil. LiverWELL is committed to being led and informed by Aboriginal and Torres Strait Islanders on bridging health outcomes for communities and improving liver health.